Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipindupindu kimepungua Haiti licha ya vifo 4000:WHO

Kipindupindu kimepungua Haiti licha ya vifo 4000:WHO

Idadi ya waliokufa kutokana na kipindupindu Haiti hadi sasa kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO ni 4,030, visa vilivyoripotiwa tangu kuzuka kwa ugonjwa huo Oktoba mwaka jana ni 210,000.

WHO inasema hata hivyo mlipuko wa ugonjwa huo unaanza kudhibitiwa na idadi ya wagonjwa wapya wanaoarifiwa kila siku ni ndogo kuliko siku za nyuma. Shirika hilo linasema wakati mijini hali ikitengamaa, vijijini maambukizi mapya yanaongezeka kutokana na huduma mbovu za afya, na taarifa duni za kuzuia kipindupindu.

WHO linasema idadi ya wagonjwa wanaolazwa hospitali sasa ni 7000 kwa wiki. Wakati huohuo shirika hilo linasema limeanza uchunguzi wa visa vinne vya kupooza vilivyowapata wagonjwa wa kipindupindu kwenye mji wa Kaskazini Magharibi wa Port de Paix, na linadhani kupooza huko ni matokeo ya dawa au chakula na sio polio. Hata hivyo kama hatua za tahadhari chanjo ya polio imeongezwa katika kampeni zinazoendelea kwenye eneo hilo.