Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano baina ya waasi na wanajeshi wa serikali yasita Darfur

Mapigano baina ya waasi na wanajeshi wa serikali yasita Darfur

Mapigano makali yaliyotokea katika jimbo linalokubwa na mzozo la Darfur nchini Sudan kati ya wanajeshi wa serikali na waasi yamepungua lakini hata hivyo hali ya wasiwasi bado inaripotiwa na kuna hofu ya kutokea kwa mapigano tena.

Mkuu wa kikosi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika AU cha UNAMID Ibrahim Gambari anasema kuwa mapigano hayo yamewalazimisha karibu watu 43,000 kukimbia makwao. UNAMID kikosi kilicho na zaidi ya wanjeshi 20,000 kilibuniwa mwaka 2008 kusaidia kumaliza vita ambavyo vimesababisha vifo vya watu 300,000 na kusababisha wengine milioni 2.7 kukimbia makawao tangu mwaka 2003. George Njogopa na taarifa kamili

(RIPORT YA GEORGE NJOGOPA)

Vikosi hivi vya kimataifa UNAMID vimeimarisha hali ya ulinzi na usalama kwa shabaya ya kudhibiti hali yoyote korofi inayoweza kuzuka upya na wakati huo huo inajenga mazingira rafiki ili kuwawezesha wakimbizi wa ndani waliokimbia makazi yao kurejea upya katika hali ya usalama na amani. Hata hivyo kwa mujibu wa Bwana Gambari vikosi vya kimataifa bado vinakabiliwa na uchache wa vitendea kazi jambo ambalo linakwamisha kwa kiwango kikubwa baadhi ya operesheni zake.

Ametaka vikundi vyote vinavyoingia kwenye mizozo kukomesha hali hiyo na akavisisitizia kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2006 baina ya serikali na kikundi cha SLA/MM juu ya usitishwaji wa machafuko.

Katika duru jingine, mwakilishi wa katibu Mkuu katika eneo hilo anayehusika na masuala ya kulinda amani Atul Khare amesema kuwa mazungumzo ya utanzuaji mzozo wa Sudan yanayofanyika huko Doha, Qatar, baina ya serikali na vikosi vya waasi sasa yameanza kupiga hatua .