Skip to main content

Kupekuwa mgari ya UM Ivory Coast ni ukiukaji wa sheria

Kupekuwa mgari ya UM Ivory Coast ni ukiukaji wa sheria

Umoja wa Mataifa umetoa onyo kwa uongozi wa Icory Coast kutosimamisha na kukagua magari ya Umoja wa Mataifa. Amri ya kufanya upekuzi ilitolewa kwa majeshi yanayomuunga mkono Rais Laurent Gbagbo kupitia vyombo vya habari vya serikali.

Bwana Gbagbo anakataa kuachia madaraka baada ya kupoteza kwenye uchaguzi mkuu na kuiacha nchi hiyo ya Afrika Magharibi katika mtafaruku mkubwa wa kisiasa. Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky anasema hatua hiyo inakiuka makubaliano baina ya Umoja wa Mataifa na Ivory Coast ya kupeleka vikosi vya kulinda amani nchini humo. Nersiky amesema,

"Nataka kuliweka bayana hili kwamba wito wa vikosi vya ulinzi na usalama vinavyomuunga mkono Bwana Gbagbo kusimamisha na kupekuwa magari ya Umoja wa Mataifa ni ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya hadhi ya majeshi ya kulinda amani (SOFA) na azimio la baraza la usalama namba 1962 la 2010 na hivyo ni kitendo kisichokubalika.

Umoja wa Mataifa unalaani kuendelea kutumia vyombo vya habari vya serikali RTI, kusambaza taarifa za uongo kuhusu mpango wa Umoja wa Mataifa UNOCI na pia kuendelea kuwa kikwazo cha shughuli za vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa katika utekelezaji wa jukumu lake kwa mujibu wa baraza la usalama.

Martin Nersiky amerejea kusema wote wanaohusika kwa mashambulizi dhidi ya raia au vikosi vya kimataifa vy kulinda amani watafunguliwa mashitaka chini ya sheria za kimataifa.