Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan imetakiwa kuwaachilia watetezi wa haki za binadamu:UM

Sudan imetakiwa kuwaachilia watetezi wa haki za binadamu:UM

Mtaalam, huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Sudan Mohamed Chande Othman leo ameelezea hofu yake juu ya serikali ya Sudan kuendelea kuwashikilia rumande watu 11 ambao ni watetezi wa haki za binadamu na waandishi habari .

Amesema wasiwasi wake ni kwamba kushikiliwa kwa watu hao kunaweza kuhusishwa na shughuli zao za kupigania haki za binadamu , amesema Sudan imeridhia mkataba wa kimataifa wa haki za kisiasa na kiraia ambao unatatoa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kutokamatwa na kuwekwa mahabusu kwa kuonewa. George Njogopa na taarifa kamili.

(SAUTI YA GEORGE NJOGOPA)

Maafisa wa usalama nchini humo waliwatia mbaroni waandishi 11 mapema mwezi uliopita na imeendelea kuwashikilia hadi sasa. Serikali hiyo imeshindwa kubainisha makosa yao mbali ya kuendelea kuwashikilia na kuwanyima mawasiliano na sehemu nyingine.

Kundi la wataalamu wa haki za binadamu lililotembelea nchi hiyo hivi karibuni limetaka Sudan kuheshimu majukumu ya kimataifa. Kundi hilo limesema serikali ya Sudan inapaswa kuwapeleka mahakamani waandishi hao kujibu mashtaka la sivyo iwaachie huru mara moja. Wataalamu hao wameelezea pia wasiwasi wao namna haki za binadamu zinavyobinywa nchini Sudan.