Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makundi ya utamaduni yatumbuiza Goma kupinga ukatili wa kimapenzi:UNHCR

Makundi ya utamaduni yatumbuiza Goma kupinga ukatili wa kimapenzi:UNHCR

Wacheza ngoma kutoka makundi tisa ya utamaduni ya makabila yamejumuika pamoja kutumbuiza kwa sarakasi wakiwa na lengo la kufikisha ujumbe wa kupambana na kiwango kikubwa cha ukatili wa kimapenzi na wa kijinsia Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Makundi hayo yalitumbuiza mjini Goma makao makuu ya jimbo la Kivu mwishoni mwa wiki wakiadhimisha siku 16 za kila mwaka za wanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia.

Vita katika jimbo hilo limewafungisha virago maelfu ya watu huku wanawake na wasichana wakijikuta katika ukatili wa kubakwa na ukatili mwingine kutokana na mazingira ya vita.

Msaidizi wa kamishina wa operesheni za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi Janet Lim aliyehudhuria hafla hiyo amesema UNHCR inahofia kiwango kikubwa cha ukatili wa kimapenzi nchini Congo na hasa eneo la mashariki ambako wanawake na wasichana takribani 12,000 inaaminika wamebakwa mwaka huu pekee.

Amesema UNHCR inafanya juhudi zote kukomesha ukatili huo na kuhakikisha wahusika wanafikishwa kwenye mkono wa sheria.

Kundi kubwa la utamaduni la Goma lilizinduliwa mwaka 2002 likiwa na jumla ya wanenguaji, wacheza sarakasi na waimbaji 70 wanawake kwa wanaume kutoka makundi tisa ya kikabila katika Kivu ya Kaskazini.