Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wataka kuwepo uchunguzi kubaini ubakaji uliofanyika wakati wa urejeshwaji kwa nguvu wakimbizi wa DRC toka Angola

UM wataka kuwepo uchunguzi kubaini ubakaji uliofanyika wakati wa urejeshwaji kwa nguvu wakimbizi wa DRC toka Angola

Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa amezikata mamlaka za Angola na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuanzisha uchunguzi juu ya madai kuwa kulikuwa na vitendo vya ubakaji wakati wa kuwarejesha wakimbizi wa Congo waliokuwa uhamishoni nchini Angola.

Bi Margot Wallström ambaye ni mwakilishi wa Katibu Mkuu anayehusika na vitendo vya unyanyasaji wa kingono kwenye maeneo yenye machafuko amesema kuwa anaamini mamlaka kwenye nchi zote mbili zinazingatia na kujali suala la haki za binadamu na kwa maana hiyo zitawajibika kuanzisha uchunguzi huo na kisha kuchukua mkondo wa sheria.

Kumekuwa na madai kuwa kundi kubwa la wanawake walibakwa wakati waliporejeshwa kwa nguvu kutoka Angola ambako walikuwa wakiishi kama wakimbizi na kurejea nyumbani Congo.

Afisa huyo ameeleza kuwa pamoja na kwamba hakuna maelezo ya kina yanayoweza kutosheleza wapi vitendo hivyo vya ubakaji vilifanyika na kina nani walihusika, lakini hata hivyo kuna umuhimu wa kuendesha uchunguzi ili kuweza kujibu maswali yote hayo.