Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ataka kuwepo mabadiliko kwenda kwa utawala wa kidemokrasia nchini Myanmar

Ban ataka kuwepo mabadiliko kwenda kwa utawala wa kidemokrasia nchini Myanmar

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito kwa utawala nchini Myanmar kuhakikisha kuwepo kwa mabadiliko kwenda kwa uongozi wa kidemokrasia kufuatia uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili katika taifa hilo la kusini mashariki mwa Asia.

Uchaguzi huo ambao ni wa kwanza kuandaliwa nchini Myanmar kwa muda wa miaka ishirini iliyopita ni moja wa mipango ya serikali ya kuelekea kwenye demokrasia. Kwenye taarifa iliyotolewa kupitia kwa msemaji wake Ban amesema kuwa uchaguzi huo ulifanyika katika mazingira isiokuwa na uwazi wa kutosha na wananchi wote hawakuweza kushiriki.

Sasa Ban anaamini kuwa utawala nchini Myanmar una jukumu la kutumia matokeo ya uchaguzi huo kuwa mwanzo mpya wa nchi hiyo pamoja na watu wake. Ban amesema kuwa ni lazima utawala wa Myanmar uonyeshe kuwa kura ni moja ya chombo cha mageuzi kwenda kwa serikali ya kidemokrasia , uwiano wa kitaifa na katika kuheshimu haki za binadamu.