Dola milioni 39 zahitajika kuisaidia Djibouti:UM
Umoja wa Mataifa leo umezindua ombi la msaada wa dola milioni karibu 39 kwa ajili ya Djibouti. Msaada huo utasaidia kutoa huduma za kibinadamu kwa watu 120,000 walioathirika na ukame nchini humo uliolikumba eneo la Afrika ya Mashariki tangu 2005.
Miaka mine mfululizo ya bila mvua za kutosha imesababisha njaa na ongezeko la utapia mlo hususani kwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano, kwenye maeneo ya vijijini ya nchi hiyo. George Njogopa na taarifa kamili.
(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)
Umoja wa Mataifa umesema kuwa watoto zaidi ya 25,000 nchini Djibouti wanakabiliwa na utapiamlo na hivyo umetoa rai ya kuongezwa misaada zaidi ili kunusuru maisha yao. Idadi hiyo inachukua asilimia 20 ya watoto wote waliochini ya umri wa miaka 5 nchini humo ambao wapo kwenye hatari hiyo.
Hali ya ukame iliyoikumba nchi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili, imesababisha kuharibika kwa mazao ya chakula na pia kuvuruga maeneo yanayotumiwa na wanamifugo kwa ajili ya malisho. Umoja wa Mataifa umesema kuwa itaendelea kushirikiana na taasisi za serikali na mashirika mengine ya hisani ili kukabili hali ya udharura inayohitajika sasa.