Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani shambulio la kigaidi kanisani nchini Iraq

UM walaani shambulio la kigaidi kanisani nchini Iraq

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Ad Melkert amelaani vikali shambulio la kigaidi dhidi ya kanisa la kikatoliki la Sayidat al-Nejat jana usiku mjini Baghdad.

Kwa mujibu wa duru za habari watu zaidi ya 52 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa wakati wa shughuli ya kuwaokoa waumini waliokuwa wanashikiliwa mateka ndani ya kanisa hilo. Naibu waziri wa mambo ya ndani wa Iraq Meja jenerali Hussein Kamal amesema washambuliaji sita pia wameuawa katika mtafaruku huo. Waumini takribani 100 walikuwa wanahudhuria misa ya jioni walipochukuliwa mateka na watu wenye silaha wanaoaminika kuwa wafuasi wa Al-Qaeida.

Bwana Melkert ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha, na serikali ya Iraq na pia amewatakia nafuu ya haraka waliojeruhiwa. Ametaka juhudi zifanywe na viongozi wa pande zote Iraq na kuweka makubaliano katika masuala yanayoleta utata kama kuundwa kwa serikali ili kuhakikisha raia wanaweza kulindwa.