Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya polio kuwalenga watoto milioni 72 Afrika

Kampeni ya polio kuwalenga watoto milioni 72 Afrika

Afrika wiki hii imechukua fursa muhimu ya kutaka kutokomeza kabisa ugonjwa wa polio wakati nchi 15 za bara hilo zilipozindua kwa wakati mmoja kampeni kabambe ya chanjo.

Chanjo hiyo inatazamiwa kuwafikia watoto milioni 72. Jumla ya watoa chanjo 290,000 wametayarishwa kugonga nyumba hadi nyumba kutoa matone ya chanjo hiyo ya polio kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano, umri unaotajwa kuwa kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya polio. Jayson Nyakundi na taarifa kamili.

(RIPOTI YA JAYSON NYAKUNDI)

Viongozi kutoka Afrika wameonyesha ushirikiano katika shughuli ya kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio mwaka 2009 na mapema mwaka 2010 baada ya kuripotiwa ugonjwa huo nchini Nigeria. Kufuatia kutolewa kwa chanjo hizo kusambaa kwa ugonjwa wa polio kunaripotiwa kupungua .

Nchi za Afrika magharibi zikiwemo Liberia na Mali zilishuhudia visa vichache kwa miezi mitano iliyopita wakati Nigeria nchi pekee barani Afrika ambayo inaendelea kushuhudia kusambaa kwa ugonjwa wa polio imepunguza ugonjwa huo kwa asilimia 98 kwa mwaka mmoja uliopita.

Nchi zote za Afrika magharibi zitaendesha kampeni ya chanjo ya ugonjwa huo mwezi Februari na Machi mwaka 2011 Kufuatia kuripotiwa visa 25 vya ugonjwa huo nchini Angola na kusambaa kwenda Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo sasa hali hii imezifanya nchi zingine za Afrika kuwa hatarini.