Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapiganaji wa zamani Sudan kurejea maisha ya kawaida

Wapiganaji wa zamani Sudan kurejea maisha ya kawaida

Maelfu ya wapiganaji wa zamani wanashiriki kwenye mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuwarejesha wapiganaji hao kwenye maisha ya kawaida Kusini mwa Sudan.

Mpango huo unaoitwa msukumo wa kupokonya silaha umeshuhudia wapiganaji saba wanaume wa zamani na wanawake wawili wakipokonywa silaha, kusajiliwa na kupewa vyeti wakati wa uzinduzi wa mpango huo kwenye mji wa Torit jimbo la Equatoria Kusini mwa Sudan.

Watu hao ni wa kwanza katika jumla ya wapiganaji wa zamani 2600 wanaotarajiwa kupokonywa silaha kwenye mpango huo unaoendeshwa na kitengo cha Umoja wa Mataifa cha upokonyaji silaha,na urejeshaji wapiganaji katika maisha ya kawaida (DDR) ambacho kinahusisha mpango wa Umoja wa Mataifa Sudan UNIMIS, shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, shirika la mpango wa chakula WFP na shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA.

Hatua ya kuwapokonya silaha wapiganaji wa zamani ilianza mapema mwaka jana nchini Sudan kama sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya amani ya 2005 CPA, ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya Kaskazini na Kusini.

Baada ya kupokonywa silaha, kufanyiwa uchunguzi wa afya na kupata ushauri nasaha wapiganaji hao wa zamani watajumuishwa kwenye jamii kwa kupewa mafunzo ya biashara na mafunzo ya ufundi kama uwashi, ushonaji, ufundi magari, udereva, ufindi bomba na ufundi mwingine.