Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa kuwarejesha wakimbizi wa DRC kutoka Zambia ni mafanikio:UNHCR

Mpango wa kuwarejesha wakimbizi wa DRC kutoka Zambia ni mafanikio:UNHCR

Shirika la Umoja la kuhudumia wakimbizi UNHCR linajiandaa kufunga kambi mbili za wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nchini Zambia.

Shirika hilo linasema hii ni kutokana na mpango maalumu wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao kufanikiwa kwa kiasi kikubwa na hadi sasa wakimbizi 40,000 wamerejea nyumbani Congo. Kambi ya Mwange itafungwa Jumanne ijayo na kambi ya Kala itafungwa mwezi ujao na mpango huo wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi kwa hiyari utakamilika mwishoni mwa mwaka.

UNHCR inasema wakimbizi wengine watakaokuwa wamesalia ambao hawataki kurudi nyumbani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo watahamishiwa kituo cha wakimbizi cha Maheba kwenye jimbo la Kaskazini Magharibi mwa zambia.

Shirika hilo linasema wanaofika nyumbani hasa wengi katika jimbo la Katanga UNHCR na washirika wake wa misaada wanatoa mafunzo ya miradi mbalimbali ya kuwasaidia wakimbuzi hao kiuchumi, pia wanapewa msaada wa chakula, malazi na usafiri.