Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haiti bado inakabiliwa na changamoto kubwa:Ban

Haiti bado inakabiliwa na changamoto kubwa:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ingawa kuna hatua kubwa zilizopigwa katika ujenzi mpya wa Haiti miezi mianane baada ya tetemeko la ardhi, bado kuna changamoto kubwa.

Ban akiwasilisha ripoti yake kuhusu mpango wa Umoja wa Mataifa Haiti MINUSTAH amesema hivi sasa nchi hiyo inaingia kipindi cha mabadiliko ambacho ni muhimu sana kwa mustakhbali wa Haiti. Amesema changamoto kubwa ukiacha ujenzi mpya ni maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge ambao ni lazima uwe huru na wa haki.

Amesema nchi hiyo kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa imefanikiwa kuepuka janga lingine kubwa la kuzuka machafuko licha ya kwamba hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii bado ni mbaya na maelfu kuendelea kuishi makambini kwa mwaka mwingine.

Amesema kutokana na hali hiyo mtihani mkubwa kwa serikali ya Haiti hivi sasa ni kuwapa makazi ya kudumu mamilioni ya wakimbizi wa ndani, ambao wengi wamepoteza nyumba zao, wengine hawawezi kulipa kodi na wale ambao hawakuwa na nyumba kabisa hata kabla ya tetemeko.