Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la kimataifa la maendeleo limesisitiza nia ya kukuza uchumi :

Kongamano la kimataifa la maendeleo limesisitiza nia ya kukuza uchumi :

Kongamano la 11 la dunia la maendeleo kwa kuuza bidhaa nje WEDF limemalizika leo mjini Geneva.

Kongamano hilo lililokusanya pamoja wajumbe zaidi ya 300 kutoka nchi 60 limeelezea matumaini kuhusu kukuwa kwa biashara baada ya kipindi cha mtikisiko wa uchumi na kurejea kusisitiza nia yake ya kutumia mfumo wa kukuza uchumi unaochagizwa na kusafirisha bidhaa nje.

Katika siku mbili za kongamano hilo mada mbalimbali zimejadiliwa zikiwemo hali sasa ya biashara ya dunia, kuinua kiwango cha ushindani kwa kutumia njia za ubunifu wa kifedha, mfumo wa sasa wa usambazaji wa dunia, umuhimu wa ubia wa mafanikio ya biashara, viwango vinavyochipuka vya sekta binafsi na athari zake kwa biashara, haja ya kuwawezesha wanawake katika biashara ili kuinua biashara na pia kuona mbele kwa kuwa na mipango ya muda mfupi na muda mrefu.

Bwana Long Yontu katibu mkuu wa kituo cha utafiti cha Uchina cha G20 amesema licha ya kukosolewa na baadhi ya mataifa yaliyoendelea, uamuzi wa Uchina kuendelea kutegemea kuuza bidhaa zake nje utaendelea, kwani amesema nchi hiyo inahitaji kufanya hivyo ili kuchagiza ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini.

Naye mkurugenzi mtendaji wa ICT Patricia R. Francis katika tamko lake la kufunga mkutano amesema ni muhimu wameona kuna dalili nzuri ya kutengamaa kwa uchumi. Lakini amesema mkutano huo umehitimisha kwamba utandawazi wa dunia hauajafikia kiwango ambacho wengi wanakifikiria na hii inamaanisha kwamba kuna fursa nzuri za biashara za kuzifanyia kazi.Amesema nchi ambazo uchumi wake unachipukia zinahitaji kulinganisha mzani wa ukuaji wa mahitaji ya ndani na kuimarisha usafirishaji bidhaa nje.