Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajira lazima iwepo kuinua uchumi ILO na IMF

Ajira lazima iwepo kuinua uchumi ILO na IMF

Shirika la kazi duniani ILO na shirika la fedha duniani IMF leo wanafanya mkutano wa siku moja mjini Oslo kujadili njia ya kuchagiza upatikanaji wa ajira baada ya msukosuko wa uchumi ulioikumba dunia.

Akizungumza katika mkutano huo mkurugenzi wa IMF Dominique Strauss-Kahn amesema analishukuru shirika la ILO kwa kusaidia kuandaa mkutano huo. Amesema hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano baina ya mashirika hayo mawili.

Bwana Kahn amesema hii ni mara ya kwanza IMF na ILO wanaungana kwa njia hii. Ameongeza kuwa wakati mwingine mashirika hayo mawili yanakuwa na mitazamo tofauti lakini wana lengo moja, ambalo ni kuwa na dunia bora kwa wote. Ameongeza kuwa nia kubwa ya ILO sio tuu katika masuala ya ajira bali pia katika kukua kwa uchumi, sawa na IMF ambayo malengo yake sio tuu katika uchumi bali pia katika masuala ya ajira.