Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cape Verde iko tayari kugawa chakula mashuleni:WFP

Cape Verde iko tayari kugawa chakula mashuleni:WFP

Baada ya miaka zaidi ya 30 ya ushirikiano na shirika la mpango wa chakula duniani WFP serikali ya Cape Verde leo imechukua jukumu kamili la mpango wa kitaifa wa kugawa chakula mashuleni.

WFP inasema hatua hiyo ni mfano kwa mataifa mengine yanayoendelea kufuata nyayo. Mpango wa kutoa chakula mashuleni kisiwani Cape Verde ulianza mwaka 1979 baada ya kisiwa hicho kupata uhuru wake mwaka 1975.

Kwa miaka yote hiyo Cape Verde imekuwa ikilitegemea shirika la WFP kwa msaada wa fedha, ueneshaji wa mpango huo na masuala ya kiufundi.Tangu mwaka 2007 serikali ilianza kuchukua udhibiti na utawala wa mpango huo kwa kuanza na asilimia 15 na mwaka huu wameweza kuendesha mpango huo kwa asilimia 100.

Mkurugenzi mkuu wa WFP Josette Sheeran katika hafla maalumu kwenye makao makuu ya WFP mjini Roma amesema chakula kwa watoto kinasaidia kuimarisha lishe yao ambayo ni kiungo kikubwa kwa maendeleo, na ameipongeza Cape Verde kwa hatua hiyo na kusema ni mfano wa kuigwa duniani kote.