Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jimbo la Equateur DR Congo lakumbwa na mafuriko, msaada wahitajika

Jimbo la Equateur DR Congo lakumbwa na mafuriko, msaada wahitajika

Eneo la Basunkusu kaskazini mwa jimbo la Equateur nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limeathirika vibaya na mafuriko.

Mratibu wa misaada ya kibinadamu kwa Afrika ya Magharibi Fidele Sarassoro amesema msaada wa haraka unahitajika . Mafuriko hayo yanafuatia mvua kubwa zilizoanza kunyesha tangu wiki jana. Nyumba 300 zimesombwa na kuwaacha watu 1500 bila makao. Vyoo vimebomoka na kuchafua maji hivyo kuongeza hatari ya magonjwa ya mlipuko ameonya Dr Issaka Compaore mwakilishi wa shirika la afya duniani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Na kutokona na nyumba nyingi kutokuwa imara mashairika ya misaada yanahofia kuwa watu wengi zaidi watapoteza makazi. Waathirika wanahitaji msaada wa haraka wa chakula, malazi, madawa, vifaa vya kupikia na maji safi. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF tayari zimepeleka msaada wa dawa za kusafishia maji ya kunywa, vifaa 100 vya dharura vya kupikia, huku WHO na UNFPA wamewasilisha kilo 300 za vifaa vya matibabu na dawa. Nalo shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR zimewasilisha msaada wa mablanketi 500 na vyandatua vya mbu.