Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mvua zinazuia tathmini ya uharibifu wa mafuriko nchini Pakistan:OCHA

Mvua zinazuia tathmini ya uharibifu wa mafuriko nchini Pakistan:OCHA

Mvua zinazoendelea kunyesha zinauia juhudi za jumuiya ya kimataifa ya misaada kutathimini athari zilizosababishwa na mafuriko nchini Pakistan.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA linasema mvua kubwa zilizonyesha katika siku chache zilizopita zimesababisha mafuriko kwenye maeneo mbalimbali ya Pakistan na matokeo yake watu wengi wamepoteza maisha, nyumba na mali na idadi kubwa hawana makao. Kwa mujibu wa msemaji wa OCHA Corine Momal Vanian, jimbo lililoathirika zaidi ni Khber Pakhtunkhwa, ambako watu laki nne wameathirika, ni mafuriko ambayo hawajayashuhudia tangu mwaka 1929.

Ameongeza kuwa majimbo mengine 23 pia yameathirika, ambapo barabara zinazounganisha majimbo hayo na mji wa Peshawar zimebomoka, na mto Swati umefurika kupita kiasi. Hadi sasa serikali ya Pakistan imekuwa ikigawa chakula, mahema na vitu vingine. Na katika jimbo la Baluchistan wilaya sana zimekumbwa na mafuriko na kuathiri watu 150,000.