Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amerika Kusini na Carebean yana pengo kubwa baina ya matajiri na masikini:UNDP

Amerika Kusini na Carebean yana pengo kubwa baina ya matajiri na masikini:UNDP

Ripoti mpya ya shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP inasema watu katika nchi za Amerika ya Kusini na visiwa vya Carebeani ndio walio na tofauti kubwa kabisa duniani ya utajiri na kipato.

Shirika hilo limetoa wito wa kuwepo na sera ambazo zitasaidia kukabiliana na tatizo hilo la kutokuwepo na usawa baina ya walio nacho na wasio nacho katika maeneo hayo. Ripoti hiyo mpya ya maendeleo imeongeza kuwa kutokuwepo na usawa ni tatizo sugu na linaloendelea katika maeneo ambayo uhamasishaji ni mdogo na linakuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya watu. Nchi kumi kati ya 15 ambazo hazina usawa duniani ziko katika maeneo hayo.

Ripoti hiyo pia imebaini kwamba inawezekana kupunguza pengo lililopo kwa njia ya kutekeleza sera za umma ambazo zinalengo la kuliondoa eneo hilo katika mtego wa kutokuwa na usawa. Mkurugenzi wa UNDP Heraldo Munoz amesema ripoti hiyo pia inasisitiza haja kuchukua hatua zaidi kukabiliana na umasikini, na kiwazo kikubwa ni kutokuwepo na usawa, jambo ambalo amesema lazima lipewe kipaumbele katika ajenda za sera za taifa.