Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma ya afya imezidiwa nguvu Moghadishu nchini Somalia:WHO

Huduma ya afya imezidiwa nguvu Moghadishu nchini Somalia:WHO

Shirika la afya duniani WHO limesema huduma ya afya mjini Moghadishu Somalia imezidiwa nguvu kutokana na ongezeko la wakimbizi wa ndani.

Shirika hilo linasema mfumo wa afya mjini humo umeshindwa kukabiliana na visa vya majeruhi na athari za vita. Imebainika kwamba kati ya Machi 20 na Julai 11 mwaka huu hospitali mbili za mjini Moghadishu zimearifu kupokea wagonjwa zaidi ya 1600walioa na majeraha ya silaha na yasiyo ya silaha, na robo ya wagonjwa hao ni watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.

Kwa mujibu wa msemaji wa WHO Paul Garwood pia watu karibu 50 wameripotiwa kufariki dunia katika hospitali hizo kwa kipindi hiki kifupi. Amesema hata hivyo idadi kamili ya waliokufa kutokana na majeraha haijulikani na cha kusikitisha zaidi idadi kubwa ni watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.