Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNDP aipongeza Ghana kwa hatua zilizopiga kuwawezesha wanawake

Mkuu wa UNDP aipongeza Ghana kwa hatua zilizopiga kuwawezesha wanawake

Mkurugenzi wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Matifa UNDP Helen Clark ameipongeza Ghana kwa hatua iliyopiga katika kuwawezesha wanawake na usawa wa kijinsia.

Amesema hiyo ni moja ya malengo manane ya maendeleo ya milenia ambayo viongozi wa dunia wameahidi kuyafikia ifikapo mwaka 2015. Bi Clark ambaye yuko nchini Ghana kwa ziara ya siku tatu amesema amefurahishwa na mambo mengi yanayompa fursa mwanamke.

Ameongeza kuwa miongoni mwa mambo hayo ni kupitishwa kwa sheria ya ukatili dhidi ya wanawake hapo 2007, ambayo ilikuwa ni mpango ulioungwa mkono na UNDP, na kuanzisha kituo cha msaada kwa wanawake waliotendewa ukatili, kituo ambacho kiko ndani ya idara za polisi.

Ghana pia imepiga hatua kubwa katika masuala ya elimu kwa kuanzisha mabweni kwa wasichana ili wakae shuleni, kugawa vifaa na sare za shule kwa wasichana wasio na uwezo na pia kugawa chakula cha bure.

Bi Clark amekutana na viongozi wanawake mjini Accra wakiwemo mawaziri na wakurugenzi. UNDP imekuwa ikiisaidia nchi hiyo kuwawezesha wanawake kuingia katika siasa na kushika nyadhifa za serikali.