Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa Darfur umekatili maisha ya watu 200 Juni pekee:UNAMID

Mgogoro wa Darfur umekatili maisha ya watu 200 Juni pekee:UNAMID

Vikosi vya kulinda amani vya muungano wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kwenye jimbo la Darfur Sudan UNAMID vimetoa ripoti na kusema idadi ya waliokufa Darfur mwezi Juni ni 221.

Ripoti hiyo inasema vifo hivyo vimesababishwa na vita, uhalifu na mapigano ya kikabila. Mapigano baina ya makabila ya Rizeigat na Misseriya mwezi jana pekee yameuwa watu 140, lakini UNAMID inasema kwa sasa hakuna mapigano zaidi tangu makundi hayo yalipotia saini mkataba wa amani Juni 28.

Katika miaka saba iliyopita inakadiriwa kuwa watu 300,000 wameuawa na wengine milioni 2.7 wameachwa bila makazi na kuwa wakimbizi kutokana na mapigano baina ya waasi na vikosi vya serikali vinavyosaidiwa na wanamgambo wa Janjaweed kwenye jimbo la Darfur. Pande zote zinashutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.