Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama ya ICC imetupilia mbali rufaa ya muaasi wa DR Congo

Mahakama ya ICC imetupilia mbali rufaa ya muaasi wa DR Congo

Majaji katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC leo wametupilia mbali rufaa ya kiongozi wa wanamgambo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Germain Katanga aliyetaka kesi ya uhalifu wa vita dhidi yake ifutwe.

ICC inasema kesi ya Bwana Katanga ambaye ni kamanda wa kundi la wapiganaji wa Ituri la FRPI itaendelea na anakabiliwa na makosa matatu ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na sita ya uhalifu wa vita baada ya kushambulia kijiji cha Bogoro kwenye jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mamia ya watu waliuawa katika shambulio hilo la Februari 2003 na wanawake wengi walilazimishwa kuwa watumwa wa ngono.

Katanga katika kesi hiyo yuko na kiongozi mwingine wa waasi Mathieu Ngudjolo Chui kamanda wa zamani kundi la FNI, ambaye anakabiliwa na makosa matatu ya ukatili dhidi ya ubinadamu na makosa sita ya uhalifu wa kivita, pia anadaiwa kubeba jukumu kubwa la kuandaa na kutekeleza shambulio la Bogoro. Tarehe 30 Juni mwaka 2009 bwana Katanga alikata rufaa ya kuomba kwamba kushikiliwa kwake tutangazwe kuwa ni kinyume cha sheria. Na Novemba 2009 mahakama ilikataa ombi hilo na kusema limechelewa kuwasilishwa kwa miezi saba.