Mahakama ya ICC yatoa kibali cha pili cha kukamatwa Rais Al Bashir
Leo kitengo cha kesi cha mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC kimetoa kibali cha pili cha kukamatwa Rais wa Sudan Omal Al Bashir.
Kibali hicho kimetolewa kwa kuzingatia kwamba kuna sababu za msingi za kuamini Rais Bashir anawajibika kwa makosa matatu ya mauaji ya kimbari yaliyofanyika dhidi ya makundi ya kikabila ya Fur, Masalit na Zaghawa. Makosa hayo ni pamoja na kimbari kwa kuuwa, kimbari kwa kujeruhi kimwili na kiakili na kimbari kwa kuchochea kwa makusudi kwa kila kundi hali ambayo ilisababishwa kusambaratika kwa makundi hayo.
Kwa mujibu wa ICC kibali hiki hakichukui wala kufuta nafasi ya kibali cha kwanza kilichotolewa dhidi ya Rais Bashir tarehe 4 Machi 2009 ambacho bado kinaendelea kufanya kazi. Kibali hocho cha kwanza kilitolewa kwa kuamini kuwa Rais Bashir anawajibika kwa makosa matano ya ukatili dhidi ya ubinadamu ambayo yanajumuisha mauaji, kuangamiza, kuwahamisha kwa nguvu, utesaji na ubakaji. Na makosa mawili ya uhalifu wa vita ambayo ni kuwashambulia kwa makusudi raia na utekaji nyara.