Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM unasema Sudan lazima ihakikishe watu wote wanashiriki uchaguzi

UM unasema Sudan lazima ihakikishe watu wote wanashiriki uchaguzi

Zaidi ya asilimia 70% ya idadi ya watu kwenye jimbo la Dafur wamejiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini Sudan mwezi wa Aprili.

Uandikisha wapiga kura uliofanyika kwa amani na utulivu mwezi Novemba na Desemba mwaka jana ni moja ya maendeleo ya kutia moyo katika jimbo hilo lililoghubikwa na machafuko, amesema Dmitry Titov ambaye ni msaidizi wa katibu mkuu kwenye masuala ya utawala wa sheria na kulinda amani, alipotoa taarifa leo kwenye baraza la usalama .

Hata hivyo kutokana na takwimu zilizoko kwenye tume ya taiafa ya uchaguzi inaonekana kwamba ni idadi ndogo sana ya wakimbizi wa ndani wamejiandikisha. Taarifa zinasema idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani wanaomuunga mkono Abdul Wahid wamegomea shughuli ya uandikishaji.

Abdul Wahid kutoka jamii ya Fur anachukuliwa kama ni mtu maarufu miongoni mwa viongozi wa waasi Dafur. Bwana Titov anasema tume ya taifa ya uchaguzi ilishindwa kuunda vituo vya uandikishaji katika baadhi ya makambi ya wakimbizi wa ndani ikiwa ni pamoja na Kalma kusini mwa Dafur.

Ameongeza kuwa serikali ya umoja wa kitaifa lazima ichukue hatua madhubuti kuhakikisha kunafanyika uchaguzi huru, wa haki na usio na dosari, ukijumuisha ushiriki wa watu walioathirika na mapigano.