Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya mzozo wa Sahara magharibi yameanza

Mazungumzo ya mzozo wa Sahara magharibi yameanza

Mzunguko mwingine wa mazungumzo yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kati ya pande zinazohasimiana Sahara Magharibi yameanza leo hapa New York. Mazungumzo hayo ya siku mbili kuhusu mpaka unaogombewa, baada ya kuzuka mapigano baina ya Morocco na frente Polisario baada ya uongozi wa kikoloni wa Hispania Sahara Magharibi kwisha mwaka 1976 yameanza Armonk hapa New York.

Yakisimamiwa na mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu bwana Christopher Ross, mazungumzo hayo yanafanyika kwa kuzingatia azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa namba 1871 la Aprili mwaka jana, ambalo lilichagiza pande husika kuafikiana kufanya mazungumzo yasiyo rasmi katika kujiandaa na duru ya tano ya majadiliano.