Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia masikini Burundi watasaidiwa na UM kupata vitambulisho vya kura bila malipo

Raia masikini Burundi watasaidiwa na UM kupata vitambulisho vya kura bila malipo

Raia wa Burundi milioni moja, waliotimia umri wa kupiga kura, watafadhiliwa bure vitambulisho vya uraia vitakavyowaruhusu kushiriki kwenye uchaguzi utakaofanyika nchini mwao mnamo mwezi Mei 2010.

 Kadhia hii ni miongoni mwa shughuli zinazoungwa mkono na Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) pamoja na mashirika mengine ya kimataifa, huduma zinazotumiwa kuhakikisha uchaguzi ujao utakuwa wa mafanikio. Katika miaka ya nyuma, kwa sababu ya gharama kubwa za kusimamia uchaguzi na ucheleweshaji wa kura, ilikuwa ni shida kwa raia masikini kupata vitambulisho vya kuwawezesha kupiga kura. Mwakilishi Mtendaji wa KM katika Burundi, Youssef Mahmoud alionya karibuni, vilevile, ya kuwa ukosefu wa fedha, kwa ujumla, unahatarisha kuzorotisha "maendeleo muhimu" ya kuleta utulivu na amani yalioshuhudiwa nchini kufuatia miongo kadha ya mapigano ya makundi ya kikabila. Kampeni ya kuwapatia raia masikini vitambulisho inalenga kusaidia zaidi raia wanawake wanaoishi kwenye vijiji, pamoja na makundi ya hali ya chini kijamii na wale raia waliopo maeneo ya mbali. Kikawaida, kwa mujibu wa taarifa ya UNDP, kitambulisho huchukua siku moja kutayarishwa na kukabidhiwa raia husika. UNDP imesaidia kihali vituo vinavyotoa vitambulisho kwenye manispaa 129, taasisi ambazo vile vile zilishafadhiliwa vifaa vinavyotakiwa kuhudumia uchaguzi. Mwaka 2010 utawasilisha duru muhimu ya maendeleo nchini Burundi, na itakuwa ni mara ya kwanza kwa uchaguzi kufanyika na kukamilishwa bila ya fujo na wala vurugu.