Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu lafanikiwa kupitisha bajeti la 2010-2011 kwa shughuli za UM

Baraza Kuu lafanikiwa kupitisha bajeti la 2010-2011 kwa shughuli za UM

Alkhamisi iliopita, Baraza Kuu la UM lilifanikiwa kupitisha bajeti la UM kwa miaka miwili ijayo, miaka ya 2010-2011, bajeti ambalo linagharamiwa dola bilioni 5.16.

Kitendo hiki kilipongezwa na KM Ban Ki-moon kuwa kilikamilishwa kwa wakati, kabla ya Baraza Kuu kumaliza shughuli zake kwa mwaka 2009. Kwa mujibu wa Msemaji wa KM, KM mwenyewe aliahidi "mchango wa bajeti liliopitishwa na Kamati ya Tano, kutumiwa kutekeleza shughuli za UM, utatetekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu kabisa." KM alimshukuru Raisi wa kikao cha mwaka huu, cha 64, cha Baraza Kuu, Dr. Ali Treki wa Libya kwa uongozi wake madhubuti uliohakikisha bajeti lilipitishwa kwa wakati. Kadhalika, KM alipongeza mchango wa Mwenyekiti wa Kamati ya Tano ya Baraza Kuu (Kamati ya Bajeti na Utawala) kwa kuyaongoza majadiliano ya Kamati kwa busara, na vile vile aliwashukuru wajumbe walioshiriki kwenye vikao kadha wa kadha vya Baraza Kuu katika mwaka 2009. Mchango wao, alitilia mkazo KM, umethibitisha wazi kwamba Mataifa Wanachama yamejifunga kuhakikisha "UM utajaaliwa hali njema ya kifedha kuendesha shughuli zake".