Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwanaharakati wa mazingira Kenya atawazwa na KM kuwa Mjumbe wa Amani mpya kwa UM

Mwanaharakati wa mazingira Kenya atawazwa na KM kuwa Mjumbe wa Amani mpya kwa UM

Ijumanne alasiri, KM Ban Ki-moon, alimjulisha rasmi mjini Copenhagen, kwenye Mkutano wa COP15, Profesa Wangari Maathai wa kutoka Kenya, kuwa ni Mjumbe wa Amani mpya wa UM, atakayehusika na masuala yanayoambatana na hifadhi ya mazingira na udhibiti manufaa wa mabadiliko ya hali ya hewa katika dunia.

KM alisema kwenye taadhima hiyo Profesa Maathai ni mwanamazingira asioweza kufananishwa, mwanaharakati wa haki za wanawake, aliye mbunge na vile vile mpokeaji wa Tunzo ya Amani ya Nobel. Alisema Wangari Maathai ni mfano hai unaothibitisha kihakika kwamba mwanadamu binafsi ana uwezo wakuleta mabadiliko yenye natija, pindi akijaaliwa hamasa na bidii ya kuimarisha maisha bora kwa wanadamu wenziwake duniani. Alikumbusha KM ya kuwa kwa miaka 45, Profesa Maathai alijitolea binafsi kurekibisha, na kufanya bora, sura na mandhari ya nchi pamoja na jamii kwenye bara la Afrika.