Skip to main content

UNICEF inasema watoto wanavia kwa sababu ya upungufu sugu wa chakula

UNICEF inasema watoto wanavia kwa sababu ya upungufu sugu wa chakula

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) nayo pia imewasilisha ripoti maalumu inaozingatia athari za ukosefu wa chakula kwa watoto wachanga.

Ripoti imekadiria watoto milioni 200, walio chini ya umri wa miaka mitano, katika nchi zinazoendelea, huwa wanateseka hivi sasa na tatizo la kuvia, yaani ukosefu wa kufikia kiwango cha kawaida katika kukua kwao. Ripoti ilisema tatizo hili husababishwa na ukosefu wa chakula cha kutosha kwa mama mjamzito na pia chakula haba kwa mtoto mdogo, hali ambayo ndio husababisha thuluthi moja ya jumla ya vifo vyote vya watoto wa chini ya miaka mitano. Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Ann Veneman, alihadharisha kwamba ukosefu wa chakula cha kutosha humnyima mtoto mchanga nguvu na huwa rahisi kwao kuambukizwa maradhi ambayo, kikawaida, yangeweza kuzuilika pindi mtoto huyo huwa anapatiwa chakula cha kutosha. Aliongeza kusema Veneman ya kuwa watoto wanaonusurika na usumbufu wa ukosefu wa chakula mara nyingi huwa na afya dhaifu ya viungo kwenye maisha yao yote, hali ambayo hudhuru vile vile uwezo wao wa kufahamu na kuelewa mambo.