Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO kuanzisha mashauriano ya kubuni miongozo halisi juu ya umiliki bora wa mali ya asili

FAO kuanzisha mashauriano ya kubuni miongozo halisi juu ya umiliki bora wa mali ya asili

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limeanzisha mashauriano ya awali kihistoria, na wadau kadha wa kimataifa kusailia miongozo inayohitajika kimataifa juu ya udhibiti bora wa umiliki wa ardhi na rasilmali nyengine za kimaumbile, mathalan, maji safi, rasilmali ya uvuvi na mali ya asili ya misitu.

Mashauriano haya ya kuweka msingi wa mapatano juu ya miongozo husika miongoni mwa wanachama wa jumuiya ya kimataifa na serikali zao, yanatarajiwa kuchukuwa zaidi ya mwaka mmoja kukamilishwa. Taasisi zitakazohusishwa na kadhia hii zitajumlisha sekta ya binafsi, serikali, wakulima maskini, makundi ya wenyeji wa kiasili, pamoja na wenye madaraka ya jamii za kienyeji, na pia wanataaluma na wataalamu huru, na mashauriano haya yatasimamiwa na kuongozwa na ofisi ya makao makuu ya shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) yaliopo Roma, Utaliana.