Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

"Wakati umewadia, kuharakisha utekelezaji wa lengo la tano la MDGs, na kupunguza vifo vya uzazi", asema Mkuu wa UNFPA

"Wakati umewadia, kuharakisha utekelezaji wa lengo la tano la MDGs, na kupunguza vifo vya uzazi", asema Mkuu wa UNFPA

Ijumatatu kwenye mji wa Addis Ababa, Ethiopia, kulifanyika Mkutano wa Wadhifa wa Juu kuzingatia maendeleo katika utekelezaji wa suala la tano la Malengo ya Maendeleo ya Milenia ya kupunguza umaskini na ufukara katika mataifa yanayoendelea.

Thoraya Obaid, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu (UNFPA) alisema kwenye risala yake kwamba mkusanyiko wao ulifanyika kwa sababu moja tu, nayo ni "kuendeleza huduma bora za uzazi kwa mama wajawazito". Alisema kwa miaka mingi wanawake wajawazito walikuwa wakifariki, kwa sababu, kwa miaka mingi, maisha yao, pamoja na matarajio ya kuwa na maisha bora, ikichanganyika na haki za kimsingi ni mambo ambayo "yalipuuzwa na kutopewa usikizi unaostahili" na jamii ya kimataifa. Alikumbusha kwamba vifo vya uzazi na ulemavu ni miongoni mwa matatizo magumu kabisa yanayofungamana na suala la uadilifu, shughuli za maendeleo na haki za binadamu katika karne ya ishirini na moja. Alikumbusha kwamba haijuzu kamwe katika ulimwengu wa sasa hivi, kwa mwanamke kufariki wakati anajifungua na kuhuisha mwana, na si haki kwa mwanmke pia kufariki kwa sababu ya utoaji mimba usio salama. Hata hivyo, Mkuu wa Taasisi ya UNFPA alisema ana matumaini hali hiyo itarekibishwa kwa natija zitakazonufaisha fungu kubwa la wanawake wa ulimwengu, kwa sababu, alitilia mkazo, masuala yanayohusu afya ya wanawake hivi sasa yamepewa uangalifu na usikizi mkubwa na jamii ya kimataifa, tukilinganisha na miaka michache iliopita, mwelekeo ambao unaashiria hatua ya kutia moyo katika kusukuma mbele maendeleo ya wanawake, kwa ujumla. Mkutano wa Addis Ababa uliandaliwa bia na UNFPA pamoja na Waziri wa Uholanzi juu ya Masuala ya Ushirkiano wa Huduma za Maendeleo na Serikali ya Ethiopia ndio iliokuwa mwenyeji wa mkutano.