Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya WHO imethibitisha 'mamilioni ya vifo vya mapema huzuilika kukiimarishwa afya ya msingi'

Ripoti ya WHO imethibitisha 'mamilioni ya vifo vya mapema huzuilika kukiimarishwa afya ya msingi'

Ripoti mpya iliochapishwa siku ya leo na Shirika la Afya Duniani (WHO) ilieleza kwamba mamilioni ya vifo vya kabla ya wakati duniani vinaweza kuzuiliwa, kwa kushughulikia mapema matatizo ya aina tano yenye kuhusu afya.

Matatizo matano haya yanajumuisha suala la uzito pungufu kwa watoto wachanga, kujamiana kusio salama, ukosefu wa maji safi, na ukosefu wa usafi wa nafsi na mazingira, na vile vile tatizo la shinikizo la damu. Ripoti yenye mada isemayo Hatari Inaokabili Afya ya Dunia ilikumbusha matatizo haya matano hujumlisha robo moja ya vifo milioni 60, vinavyokadiriwa kutukia kila mwaka ulimwenguni. Ripoti ilifafanua vipengele 24 vinavyoathiri afya, ikichanganyisha masuala yanayohusu mazingira, tabia haribifu za wanadamu na fiziolojia, mathalan, uchafuzi wa hewa, matumizi ya tumbaku na lishe ya kiwango cha chini. Ripoti vile vile ilionya kwamba utipwatipwa na uzito mkubwa kwa wanadamu husababisha vifo zaidi kuliko uzito pungufu.