Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makampuni ya bima yajiunga na UM kudhibiti 'uchumi wa kijani'

Makampuni ya bima yajiunga na UM kudhibiti 'uchumi wa kijani'

Kampuni za kimataifa za bima, zinazodhibiti rasilmali inayogharamiwa matrilioni ya dola, zimejiunga na wataalamu mashuhuri wa kimataifa kwenye uchunguzi, wenye kuungwa mkono na UM, wa kuhakikisha viwanda vinatumia utaratibu unaosarifika na usiochafua mazingira.

Taarifa hii imekaribishwa na mkuu wa shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira, Achim Steiner na vile vile Mrithi wa Ufalme wa Uingereza, Prince Charles. Huu ni uchunguzi wa kwanza kufanyika kwenye sekta ya biashara ya bima, sekta yenye nguvu na ambayo inatarajiwa kuyatekeleza majukumu muhimu ya kuharakisha mageuzi yatakayowasilisha uchumi wa dunia ulio safi, usiochafua mazingira ambapo viwanda vitapunguza, kwa kima kikubwa lile tatizo la kumwaga hewa chafu kwenye anga na kulikabili kikamilifu. Taarifa hii imetangazwa wiki sita kabla ya Mkutano Mkuu wa UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa kufanyika katika mji wa Copenhagen, Denmark. Waraka unaohusu mwelekeo mpya wa makampuni ya bima, unaozingatia dhamana ya viwanda katika kuimarisha uchumi wa mazingira ya kijani, ulitazamiwa kuwakilishwa hii leo katika mkusanyiko wa makampuni yanayohudumia shughuli za kifedha unaofanyika kwenye mji wa Cape Town, Afrika Kusini.