Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Udhalilishaji dhidi ya wanawake bado waendelezwa kwenye maeneo ya mapigano, atahadharisha ofisa wa kamati ya CEDAW

Udhalilishaji dhidi ya wanawake bado waendelezwa kwenye maeneo ya mapigano, atahadharisha ofisa wa kamati ya CEDAW

Naéla Gabr, mwenyekiti wa kamati inayosimamia utekelezaji wa Mkataba wa UM Kuondosha Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) Ijumatatu alipohutubia Baraza Kuu aliwaeleza wajumbe wa kimataifa kwamba vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji katili wa wanawake walionaswa kwenye mazingira ya mapigano bado umeselelea duniani,

na mara nyingi wakosa wa jinai hiyo huwa hawashikwi au kuadhibiwa na wenye madaraka na mamlaka. Kutokana na bayana hii, alisema kamati yake imeikaribisha, kwa ridhaa kuu, hatua iliochukuliwa na Baraza la Usalama, ya kupitisha azimio liliotilia mkazo kwamba litazingatia kuweka vikwazo ziada, vikali, vya kiuchumi na jamii, dhidi ya yale mataifa yenye mapigano ambapo wanawake na watoto wa kike huripotiwa wanakandamizwa kimabavu. Kadhalika, Bi. Gabr aliwakumbusha wawakilishi wa Baraza Kuu juu ya umuhimu wa chombo cha sheria ya kimataifa kama Mkataba wa CEDAW, chombo ambacho alisema ndicho kilisaidia kubadilisha, kwa mafanikio ya kuridhisha, maisha ya wanawake wingi ulimwenguni, na vile vile kuzilazimisha serikali kadha wanachama kugeuza sheria, sera za kitaifa na miradi ya kizalendo ili kuhakikisha wanawake huwa wanatekelezewa haki zao halali kwa kulingana na sheria za kimataifa.