Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNFCC anasema mchango ziada wa viongozi wa kimataifa unatakiwa kukamilisha Makubaliano ya Copenhagen

Mkuu wa UNFCC anasema mchango ziada wa viongozi wa kimataifa unatakiwa kukamilisha Makubaliano ya Copenhagen

Yvo de Boer, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya UM kuhusu Mkataba wa Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC) ameripoti kupatikana maendeleo ya kutia moyo, kwenye mazungumzo ya matayarisho ya waraka wa kuzingatiwa kwenye Mkutano wa Copenhagen juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Hata hivyo, De Boer alihadharisha mazungumzo yao hayatoweza kufanikiwa kuweka misingi ya kubuni mkataba mpya wa kimataifa bila ya mchango hakika kutoka viongozi wa mataifa makuu. Aliyasema hayo leo Alkhamisi kutokea Bangkok, Thailand ambapo wajumbe wataalamu wa kutoka nchi wanachama 180, wamekusanyika kutayarisha waraka utakaowasilisha itifaki ya kimataifa katika mkutano wa Disemba wa Copenhagen. De Boer aliwakumbusha wajumbe wa kimataifa kwamba wakati unawaponyoka, na kuwataka waweke kando farakano zao na kulenga majadiliano kwenye vipengele vitakavyokamilisha maafikiano ya Copenhagen yatakayoleta natija kwa umma wote wa kimataifa. Mkutano wa Bangkok, uliochukua wiki mbili, utahitimisha majadiliano yake kesho Ijumaa.