Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Liberia: KM apendekeza operesheni za amani ziongezwe mwaka mmoja zaidi

Liberia: KM apendekeza operesheni za amani ziongezwe mwaka mmoja zaidi

KM amechapisha ripoti mpya kuhusu maendeleo katika kurudisha utulivu na amani nchini Liberia, iliotolewa rasmi Ijumatatu ya leo.

Ndani ya ripoti, KM alieleza kwamba hali Liberia, kwa ujumla, bado ni dhaifu, hususan katika ujenzi wa taasisi za usalama na zile taasisi zinazowataka raia kuhishimu sheria, pamoja na kwenye uwezo wa kuzalisha ajira. Ripoti ilisisitiza kwamba taarifa mpya ya Kamisheni ya Ukweli na Upatanishi (TRC) ya Liberia iliotolewa karibuni itasaidia kusukuma mbele juhudi za raia katika kuwasilisha upatanishi wa kudumu miongoni mwa makundi yaliokuwa zamani yakihasimiana. Wakati huo huo ripoti ya KM ilisema ina wasiwasi na vitisho vya kudhuriwa, vilivyofanyiwa baadhi ya wajumbe wa Kamisheni ya TRC na watu wasiotambulika. Aliongeza kusema kwamba taasisi dhaifu za kienyeji na kitaifa huzuia serikali kukamilisha Miradi ya Kupunguza Umaskini nchini. Ripoti ya KM, kadhalika, imependekeza muda wa operesheni za ulinzi amani za shirika la UM la UNMIL, katika Liberia, uongezwe kwa mwaka mmoja zaidi mpaka Septemba 2010, hususan tukizingatia kwamba mnamo 2011 Liberia inatarajiwa kufanyisha uchaguzi mpya wa taifa.