Skip to main content

UM imelaani shambulio la majengo yake Usomali Kusini

UM imelaani shambulio la majengo yake Usomali Kusini

Ijumapili ya tarehe 16 Agosti (2009) watu saba mpaka 10, waliobeba silaha, walishambulia majengo ya Shirika la Miradiya Chakula Duniani (WFP) katika mji wa Wajiid, katika Usomali kusini, mnamo saa sita za usiku kwa majira ya Afrika Mashariki, kwa mujibu taarifa ya Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA).

Baada ya mapigano ya muda wa robo saa, iliripotiwa majambazi watatu wenye silaha waliuawa na mmoja wao alijeruhiwa vibaya na walinzi wa majengo ya UM. Taarifa iliotolewa na UM juu ya tukio hili ililaani vikali mashambulio dhidi ya majengo yake. Tukio hili ni la nne kuzuka dhidi ya majengo ya UM, katika miezi miwili iliopita. Graham Farmer, kaimu Mkazi wa UM na Mratibu wa Misaada ya Kiutu kwa Usomali alinakiliwa akisema "mashambulio haya ya moja kwa moja, na ya makusudi dhidi ya wahudumia misaada ya kiutu wa kimataifa ni vitendo visiostahamilika hata kidogo", na aliyasihi makundi husika yote kuwapataia wahudumia misaada ya kiutu nchini, uwezo unaoridhisha ili kuwafikia raia muhitaji, bila pingamizi. UM umeshatoa maonyo kadha wa kadha karibuni, kwa makundi yanayohusika na mzozo wa Usomali juu ya usalama wa wale wafanyakazi wanaohudumia misaaada ya kiutu kwa watu milioni 3.2, ambao hujumuisha asilimia 40 ya idadi ya umma wa Usomali, umma ambao umedhoofika kwa sababu ya mchanganyiko wa migogoro iliofumka nchini mwao, pamoja na ukame, bei ya juu ya vyakula na vile vile kuporomoka kwa thamani ya fedha za kizalendo.