Kuharibika ghafla kwa usalama Chad Mashariki kwaihangaisha UM
Jamii ya wahudumia misaada ya kiutu katika Chad imeripoti kushtushwa kwa kuharibika kwa ghafla hali ya usalama Chad mashariki katika wiki za karibuni.
Timu ya Watumishi wa UM Wakazi wanaohusika na Ugawaji wa Misaada ya Kiutu wamewashauri wafanyakazi wake kuchukua kila hadhari kwenye miendo yao, hususan wanapokuwa kwenye zile sehemu za Goz Beida, Kerfi na Koukou, ziliopo kilomita 100 kutoka mpaka na Sudan kwa sababu ya kufumka kwa hali ya hatari kwenye eneo lao. Wakati huo huo, UM umearifu idadi ya watu wahamaji wanaokimbia mzozo uliozuka katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao wamelekea Chad kuomba hifadhi ya kisiasa, jumla hiyo iinazidi kuongezeka. Wahamiaji 17,811 wamesajiliwa kuingia Chad kusini karibuni kutoka JAK, na kujiunga na wazalendo wenziwao 60,000 wengine waliohamia huko siku za nyuma.
KM anafuatilia maendeleo Chad mashariki, kwa wahka mkubwa, na amenakiliwa akiyasihi makundi yote yanayohasimiana kuhishimu shughuli za UM na zile za mashirika yasio ya kiserikali, katika Chad mashariki, ambazo huhusika na ugawaji wa misaada ya kiutu kwa umma muhitaji. Vile vile makundi hayo yalinasihiwa kutosambaza vikosi vyao kwenye yale maeneo ambapo operesheni za ulinzi wa Shirika la Amani la UM kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad (MINURCAT) huendelezwa. Alionya KM ya kuwa majaribio ya kuvuruga utulivu na amani ya eneo kwa kutumia mabavu, hayatoruhusiwa abadan, tukio ambalo likijiri vikosi vya MINURCAT vitalazimika kutumia nguvu, kama yalivyoishinishwa na maazimio ya Baraza la Usalama, ili kuwahifadhi raia dhidi ya mashambulio ya makundi yenye kuchukua silaha na ambayo huhatarisha usalama wa raia.