Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumbukumbu ya miaka 15 ya mauaji ya Rwanda kuadhimishwa na UM

Kumbukumbu ya miaka 15 ya mauaji ya Rwanda kuadhimishwa na UM

Kadhalika, tarehe 07 Aprili 2009 inaadhimisha miaka 15 ya mauaji ya halaiki yaliotukia Rwanda katika 1994.

 Msiba huu umeitanabahisha jumuiya ya kimataifa ya kuwa jukumu la kuzuia mauaji ya halaiki ya kijamii yasitukie ni dhamana ya walimwengu wote. Msimamo huo ulitiliwa mkazo na KM wa UM Ban Ki-moon, ambaye kwenye taarifa alowasilisha kuhusu kumbukumbu za mauaji ya halaiki Rwanda, alisisitiza kwamba kwa walimwengu "kufanikiwa, kupiga vita jinai ya halaiki, kwa uwiano na ushupavu waliodhihirisha waathirika wa maafa hayo, na kuweza kuzihishimu kidhati kumbukumbu za wale walioangamia Rwanda miaka 15 iliopita, tunawajibika kujumuisha juhudi zetu sote katika kukabiliana na msiba huu." Mnamo mwezi Aprili 1994 walimwengu walikabiliwa na janga ovu la mauaji katika Rwanda, ambapo watu 800,000 wenye jadi ya KiTutsi pamoja na wale WaHutu waliofuata mtizamo wa wastani kisiasa waliuawa, wingi wao kwa kupigwa mapanga, katika kipindi cha karibu siku 100 mfululizo. Kumbukumbu za msiba wa Rwanda katika UM zinaadhimishwa kwa mikutano, warsha na maonyesho ya picha, ambapo nchi wanachama huzinduana umuhimu wa juhudi za kipamoja za kuhakikisha janga hili halitozuka tena ulimwenguni.