Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamanda Cheka ajisalimisha DRC, UM wakaribisha

Kamanda Cheka ajisalimisha DRC, UM wakaribisha

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono kwenye mizozo bi Pramila Patten, ambaye anazuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, amekaribisha kujisalimisha hii leo kukikokuwa kukisubiriwa kwa muda mrefu kwa kamanda na mbabe wa kivita Ntabo Ntaberi Cheka.

Cheka aliyejisalimisha kwa mpango wa Umoja wa mataifa nchini DRC, MONUSCO alihusishwa na ubakaji wa kundi la raia wapatao 378 katika eneo la Walike Mashariki mwa DRC, ubakaji uliofanyika kwa muda wa siku nne kati ya Julai na Agosti 2010,ukitumika kama mbinu ya kivita na adhabu ya pamoja.

Kundi lenye silaha alilokuwa akiliongoza la Mai Mai Cheka/Nduma, limeorodheshwa katika ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kuhusika na ukatili wa kingono vitani , au kwa ubakaji na ukatili mwingine wa kijinsia. Kamanda Cheka pia aliwekwa kwenye orodha ya vikwazo ya baraza la usalama mwaka 2011 na amekuwa akikwepa mkono wa sheria kwa miaka mingi.