Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia lazima ijitahidi kulinda na kuhifadhi mikoko:UNESCO

Dunia lazima ijitahidi kulinda na kuhifadhi mikoko:UNESCO

Dunia inahitaji kufanya juhudi zaidi kulinda na kuhifadhi mikoko ya pwani ambayo ni miongoni mwa maliasili iliyohatarini duniani. Wito huo uliotolewa leo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO .

UNESCO imetoa wito huo katika siku ya kimataifa ya uhifadhi wa mfumo wa mikoko inayoadhimishwa kila mwaka Julai 26.

Mikoko, na aina zingine za miti zinazoota ufukweni mwa bahari na kwenye mito inasaidia kuimarisha uhakika wa chakula, kuendeleza uvuvi na bidhaa zingine za msituni.

Pia inajukumu muhimu na la kipekee la kukusanya na kuhifadhi kiasi kikubwa cha gesi ya ukaa kutoka hewani na baharini, ambacho ni muhimu kwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Takribani asilimia 67 ya mikoko imetoweka hivi leo na karibu mikoko yote ambayo hailindwi inaweza kutoweka katika miaka 100 ijayo. UNESCO inaitaka jumuiya ya kimataifa kubadili mwenendo huo wa uharibifu, kwa sababu ya jukumu muhimu la mikoko katika kuhakikisha dunia inakuwa na afya muafaka.