Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNECE, UNITAR zaanzisha ubia wa kutekeleza SDGs

UNECE, UNITAR zaanzisha ubia wa kutekeleza SDGs

Katika kuwezesha utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs, taasisi mbili za Umoja wa Mataifa mjini Geneva zimeanzisha ubia ili kukuza viwango na uwezo katika kufikia melengo hayo.

Taasisi hizo ambazo ni kamisheni ya uchumi ya bara Ulaya  UNECE na taasisi ya mafunzo na utafiti UNITAR kwa pamoja katika taarifa zimeeleza kuwa maeneo yatakayopewa kipaumbele  katika jitihada za pamoja ni ubia katika taasisi binafsi za umma, usalama barabarani na mazingira.

Taarifa  hiyo inasema kuwa utekelezaji wa SDGs unakabiliwa na changamoto kadhaa, mathalani uwezeshaji kifedha kwa ajili ya miundombinu mipya ya maji safi, afya, na upatikanaji wa nishati ambavyo vinahitaji takribani dola bilioni saba kwa mwaka.

Zikitolea mfano, taasisi hizo zimesema serikali hususani zile za kipato kidogo ambapo mahitaji ni ya dharura hazitakuwa na rasilimali fedha za kutosha kuziba pengo hilo licha ya misaada ya kimaendeleo. Hivyo ushirikiano wa sekta binafsi na uwezeshaji mkubwa wa kifedha utahitajika.