Mkakati mpya wa mazingira katika ulinzi wa amani wawasilishwa
Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu operesheni za ulinzi wa amani Atul Khare amewasilisha mkakati mpya wa mazingira katika uendeshaji wa operesheni za amani za Umoja wa Mataifa katika Chuo Kikuu cha Columbia hapa mjini New York Jumanne.
Bwana Khare amelezea mtazamo wa idara yake kuwa Ofisi zao kwenye maeneo mbali mbali zinawajibika kufanya kazi katika ufanisi wa kiwango cha juu katika matumizi ya mali asili, na kutohatarisha watu, jamii na mazingira popote iwezekanavyo.
(Sauti ya Atul)
"Na kulinda mazingira ni lazima tuweke maanani vitendo tunavyofanya ili kuendeleza mazingira bora. Wajibu wetu ni kuleta amani na pia kuhamasisha matumizi bora ya mazingira yetu kwa njia iliyo sawa. "
Amesema mkakati huo utachukua miaka sita kufikia dhamira hii kwa kuzingatia sera zilizopo, kujifunza kupitia mfumo wa Umoja wa Mataifa, kuhakikisha utendaji ambao ni sambamba na malengo ya maendeleo endelevu katika kulinda duniani kutokana na uharibifu na usimamizi endelevu wa mali ya asili.
Akiongezea kuwa mkakati huo utaendelea kupewa kipaumbele na kufanyika ukarabati akibainisha changamoto na nguzo tano za msingi ambazo ni nishati, maji na maji machafu, taka, madhara na mifumo ya usimamizi wa mazingira.
Malengo muhimu ya mkakati huo yanapaswa kufikia mnamo mwaka 20202. Idara yake inasaidia operesheni 36 za amani zikiwemo operesheni16 za kulinda amani na operesheni maalumu 19 za kisiasa katika nchi zaidi ya 30.