Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi lazima zichukue hatua kuhakikisha matumizi ya dawa ni salama bila madhara:WHO

Mgonjwa kiwa na sampuli ya vidonge.
UNICEF/Olivier Asselin
Mgonjwa kiwa na sampuli ya vidonge.

Nchi lazima zichukue hatua kuhakikisha matumizi ya dawa ni salama bila madhara:WHO

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa Ulimwenguni WHO limesema , nusu ya madhara yote yanayoweza kuzuilika katika huduma za afya yanahusiana na dawa, huku robo ya madhara hayo ni mabaya sana au yanayohatarisha maisha.

Onyo hilo limetolewa leo mjini Geneva Uswis katika kuelekea Siku ya usalama wa wagonjwa duniani itakayoadhimisha kesho tarehe 17 Septemba ambayo mwaka huu WHO inasisitiza kuhusu “Mzigo wa kimataifa wa madhara ya dawa”.

Kwa mujibu wa shirika hilo la wazee ni mojawapo ya makundi yaliyo hatarini zaidi ya kupata madhara ya dawa, hasa wale wanaotumia dawa nyingi.

Shirika hilo limeongeza kuwa viwango vya juu vya madhara yanayohusiana na dawa pia huonekana katika huduma za upasuaji, huduma za dharura na dawa za dharura.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema "Dawa ni zana zenye nguvu za kulinda afya. Lakini dawa ambazo zimeagizwa kimakosa, kuchukuliwa vibaya au zisizo na ubora zinaweza kusababisha madhara makubwa. Hakuna mtu anayepaswa kuumizwa wakati anatafuta huduma."

Makosa na dawa zisizo salama ni hatari kubwa

Dawa za vijiua vijasumu
World Bank/Simone D. McCourtie
Dawa za vijiua vijasumu

Takwimu za WHO zinaonyesha kwamba mazoea ya kutumia dawa zisizo salama na makosa ya utoaji dawa ni mojawapo ya sababu kuu za majeraha na madhara yanayoweza kuepukika katika mifumo ya huduma za afya duniani kote.

Gharama za kimataifa znayohusishwa na makosa ya utoaji dawa zimekadiriwa kuwa dola bilioni 42 kila mwaka.

WHO imeongeza kuwa “Hitilafu za utoaji dawa hutokea kutokana na masuala ya kimfumo na au sababu za kibinadamu kama vile uchovu, mazingira duni au uhaba wa wafanyakazi ambao huathiri kuagiza, kunukuu, kusambaza, usimamizi na ufuatiliaji. Makosa haya yanaweza kusababisha madhara makubwa, ulemavu na hata kifo.”

Siku ya usalama wa wagonjwa duniani inalenga kuongeza uelewa na ushiriki wa umma na kuhimiza nchi kukuza usalama katika huduma za afya.

Mwaka huu siku imezingatia hasa usalama wa dawa na kauli mbiu ikiwa ‘Dawa bila Mmadhara’.

Kampeni hiyo pia itaona itaenda sanjari na ujumuishaji wa changamoto ya kimataifa ya usalama wa wagonjwa ya WHO inayoendelea, ambayo ni Dawa bila madhara, kwa lengo la kupunguza madhara yanayoweza kuepukika yanayohusiana na dawa duniani kote.

Mapendekezo ya WHO

Watoto wakiwa na vidonge vyao tayari kumeza ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs
WHO
Watoto wakiwa na vidonge vyao tayari kumeza ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs

WHO inachagiza uboreshaji wa haraka katika mikakati ya kupunguza madhara yanayohusiana na dawa katika maeneo muhimu ya hatari.

Zaidi ya hayo, shirika hilo linafanya kazi na washirika wengine kuunda miongozo ya nyenzo za kiufundi za usalama wa dawa, ikijumuisha muhtasari wa sera na suluhu za usalama wa dawa kama vile usalama wa dawa kwa dawa zinazofanana na sauti zinazofanana (LASA).

Dawa za LASA zinaweza kuonekana au kutamkwa sawa, ama kwa majina yao ya kawaida, au chapa.

Pia wanaweza kuwa na ufungashaji sawa, majina ya sauti zinazofanana, au herufi zinazofanana.

WHO inasema dosari katika mifumo ya kuagiza dawa ni mchangiaji mkubwa wa madhara yanayohusiana na dawa, pamoja na makosa ya kibinadamu.

Ushahidi umeonyesha kuwa zaidi ya nusu ya madhara yote ya dawa hutokea wakati dawa zinapoagizwa na zinapochukuliwa na wagonjwa kutokana na kutokuwepo ufuatiliaji wa kutosha.

Kundi la hatari zaidi kwa madhara yanayohusiana na dawa ni viua vijasumu, lakini dawa kama vile za kutuliza au za usingizi, dawa za kuzuia uvimbe na dawa za moyo na shinikizo la damu pia huleta hatari kubwa.

WHO inatoa wito kwa wadau wote kuendeleza juhudi za kupunguza madhara yanayohusiana na dawa, kuandaa mikakati na miundo ya kuboresha usalama wa dawa katika ngazi ya ndani, kitaifa, kikanda na kimataifa, na kutoa ahadi ya kushughulikia changamoto ya kuhakikisha dawa bila madhara.