Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola sasa iko Butembo,  mashariki mwa DRC- UNICEF

Afisa wa UNICEF azungumza na watoto kuhusu umuhimu wa kuzuia Ebola karibu na Mangina, Kivu Kaskakzini ,DRC
UNICEF/Mark Naftalin
Afisa wa UNICEF azungumza na watoto kuhusu umuhimu wa kuzuia Ebola karibu na Mangina, Kivu Kaskakzini ,DRC

Ebola sasa iko Butembo,  mashariki mwa DRC- UNICEF

Afya

Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa la UNICEF linapanua wigo wa operesheni zake za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo,  DRC baada ya serikali kuthibitisha kuwepo kwa wagonjwa wapya wawili  kwenye mji wa Butembo, jimboni Kivu Kaskazini.

UNICEF inasema inatuma kikosi chake huko kufanya kazi ya kuhamasisha jamii jinsi ya kujilinda dhidi ya ugonjwa huo.

Christian Boulierac, msemaji wa  UNICEF mjini Geneva, Uswisi leo amewaambia waandishi habari kuhusu umuhimu wa mji wa Butembo akisema, “Butembo  ni mji muhimu wa kibiashara na una watu takriban milioni moja  na kwa hivyo kuna hatari ya uwezekano wa virusi vya Ebola kuenea haraka na tunatuma mjini Butembo kikosi cha wataalamu 11 wa mawasiliano kwa jamii, elimu. Usafi wa maji na kujisafi.”

UNICEF inasema ingawa visa vya Ebola ni vichache huko Butembo, ni vyema kuchukua hatua haraka iwezekanavyo kuepusha kuenea zaidi.

Halikadhalika shiriak hilo linaendelea kushirikiana na wadau wake katika sehemu zingine muhimu za Mangina na Beni jimboni humo.

Tangu mlipuko wa Ebola jimboni mapema mwezi uliopita, UNICEF imefanikiwa kufikisha ujumbe wa kukabili ebola kwa watu milioni 3.3.