Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

24 JANUARI 2024

24 JANUARI 2024

Pakua

Hii leo jaridani tunaangazia siku ya kimataifa ya elimu duniani mada kuu ikiwa ni elimu na mchango wake wa kuleta amani ulimwenguni. Makala tunakupeleka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na mashinani nchini Kenya, kulikoni?

  1. Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeyatumia maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Elimu kuangazia jukumu muhimu la elimu na walimu katika kukabiliana na kauli za chuki, jambo ambalo limekithiri katika miaka ya hivi karibuni kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii na hivyo kuharibu muundo wa jamii kote duniani.     
  2. Nchini Uganda katika makazi ya wakimbizi ya Kyangwali wilaya ya Kikuube magharibi mwa taifa hilo, suala la mchango wa elimu kwenye amani liko dhahiri kwani tulipotembelea katika makazi hayo, Yahya Kato ambaye ni Mwalimu Mkuu katika Shule ya msingi Kasonga kwenye makazi hayo ya wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Sudan aliteueleza kile wanachofanya.
  3. Makala inatupeleka huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hususan jimboni Ituri mashariki mwa nchi hiyo ambako wakazi wanazungumzia mchango wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO wakati huu ambapo ujumbe huo umeanza kufungasha virago. 
  4. Mashinani tutaelekea katika kaunti ya Garissa nchini Kenya ambapo mvua kubwa inayohusiana na El Niño, imesababisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao, kuharibu miundombinu na kusababisha kipindupindu na magonjwa mengine yatokanayo na maji yasiyo safi na salama, Mohammed Saidi, Chifu wa kambi ya waislamu waliopoteza makazi yao katika kaunti ya Garissa anasimulia kinachojiri.      

Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
9'57"