Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yawaweka katika hatari ya kukosa chanjo watoto milioni 117:UN

COVID-19 yawaweka katika hatari ya kukosa chanjo watoto milioni 117:UN

Pakua

Kutokana na taarifa iliyotolewa hii leo mjini Atlanta na New York Marekani, pamoja na Geneva Uswisi, wakati COVID-19 ikizidi kusambaa duniani, zaidi ya watoto milioni 117 katika nchi 37 wanaweza kukosa kupokea chanjo ya kuokoa maisha dhidi ya surua.

Taarifa hiyo iliyotolewa na mashirika mbalimbali yanayounda mkakati wa surua na rubella yakiwemo shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, UN Foundation, shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa na shirika la msalaba mwekundu la Marekani, imesema kampeni za chanjo ya suraa katika nchi 24 tayari zimecheleweshwa, na nyingi zaidi zitaahirishwa.

“Wakati huu wa changamoto, Mkakati dhidi ya Surua na Rubella, M&RI inashikamana na familia, jamii, serikali na wahudumu wa dharura na tunaungana na wadau wetu wa chanjo na afya wakiwemo muungano wa chanjo dunini, Gavi na mkakati wa wa kimtaifa wa kutokomeza Polio duniani GPEI katika mtazamo wetu wa pamoja na kupambana na dhidi ya tishio la COVID-19. Mlipuko wa ugonjwa huu duniani unahitaji juhudi zilizoratibiwa na kujitolea kwa rasilimali kuhakikisha wafanyakazi wa afya waliko mstari wa mbele kote duniani wanalindwa wanapokabiliana na kupambana na tishio hili jipya. Wakati huo huo, tunapaswa pia tuongoze juhudi za kulinda huduma muhimu za chanjo, hivi sasa na kwa siku za usoni.” Imesema taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa WHO imetoa mapendekezo mapya ambayo yameungwa mkono na kundi la wataalamu wa chanjo ili kuzisaidia nchi kuendeleza shughuli za chanjo wakati wa janga la COVID-19. Mapendekezo yameshauri kwamba serikali zinaweza kusitisha kwa muda mfupi chanjo katika maeneo ambayo hakuna mlipuko wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Washirika wa M&RI wanakubaliana kwa dhati  na mapendekezo haya na kwamba nchi ziendelee na utoaji chanjo  wakati zikihakikisha  usalama wa jamii na wahudumu wa afya. Pia mapendekezo yanaiomba serikali kufanya uchambuzi wa kina wanapoamua ikiwa  wasitishe chanjo wakati wa mapambano dhidi ya COVID-19. 

 

 

Audio Credit
UN News/Jason Nyakundi
Audio Duration
2'47"
Photo Credit
©UNICEF/Allan Stephen