Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikosi cha kikanda Sudan Kusini kukamilika mwishoni mwa mwaka huu- UNMISS

Kikosi cha kikanda Sudan Kusini kukamilika mwishoni mwa mwaka huu- UNMISS

Pakua

Kikosi cha ulinzi cha kikanda, RPF, kinachopelekwa nchini Sudan Kusini kitakuwa kimekamilika ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer amesema hayo hii leo akizungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu Juba, akigusia kikundi hicho kinachoundwa na askari kutoka nchi za Afrika.

Amesema kikosi hicho kilichoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kitakuwa na jumla ya askari 4,000.

(Sauti ya David)

“Kuna takribani wanajeshi 750 ambao wameshawasili. Tunasubiri waliosalia kutoka Rwanda ambao ni 900 na wengine idadi hiyo hiyo kutoka Ethiopia. Vikosi tangulizi kutoka nchi hizo mbili tayari vimewasili. Kwa hiyo kombania tatu za Ethiopia na Rwanda tayari zimewasili na waliosalia watafika kati ya sasa na krismas.”

Bwana Shearer ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS amegusia kuendelea kuzorota kwa usalama kwenye jimbo la la Torit akisema anapanga kutembelea eneo hilo ili kufuatilia mipango ya kuanzisha doria za pamoja kati ya ujumbe huo na serikali ya jimbo hilo.

(Sauti ya Shearer)

 “Nitatembelea Torit wiki chache zijazro na kupendekeza doria za pamoja au doria nyakati za usiku mtaani ili kusaidia kuimarisha ulinzi. Katu hatuwezi kuhakikisha usalama lakini wakati mwingine uwepo wa wanajeshi wa UNMISS na polisi kwenye mitaani kunaweza kusaidia kuimarisha hali ya usalama.”

Photo Credit
Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer(kushoto) akihutubia waandishi wa habari. Picha: UNMISS