MONUSCO yahimiza kuheshimu uhuru na haki ikiwataka wadau wote kujizuia na ghasia

MONUSCO yahimiza kuheshimu uhuru na haki ikiwataka wadau wote kujizuia na ghasia

Pakua

Maman S. Sidikou, mwakilishi maalimu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na mkuu wa mpango wa Umoja wa mataifa nchini humo MONUSCO, ameelezea hofu yake dhidi ya watu kukamatwa kiholea na kuwekwa rumande kunakofanyika katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo.

Amesema kamatakamata hiyo ni kufuatia asasi za kiraia kuchagiza kuandamana kwa amani dhidi ya kuchelewa kutangazwa tarehe ya uchaguzi na kutoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi mkuu kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Mnamo tarehe 31 Julai Umoja wa Mataifa uliorodhesha zaidi ya watu 120 kukamatwa au kuwekwa kizuizini mjini Kinshasa, Goma, Lubumbashi, Beni, Butembo, Bukavu na Mbandaka. Miongoni mwa walioshikiliwa ni wawakilishi wanane wa vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na mwandishi wa Radio Okapi na wengine wawili wa vyombo vya habari vya kimataifa ambao waliachiliwa baada ya MONUSCO kuingilia kati.

Umati wa watu pia ulitawanywa kwa nguvu mjini Kisangani na Bukavu baada ya posili wa taifa kutumia risasi za moto na kujeruhi watu watatu.

Sidikou amesema anatiwa hofu na vikwazo vinavyowekwa dhidi ya kukusanyika kwa amani na kukamata watu ambao wanataka kuelezea mitazamo yao ya kisiasa, pia kuwalenga waandishi wa habari na kuwapokonya vifaa vyao.

Ametoa wito kwa uongozi wa kitaifa na mashinani kudumisha haki za msingi na uhuru kama zilivyoainishwa kwenye katiba ya nchi hiyo, na wadau wote kujizuia na kukumbatia majadiliano badala ya vitendo vitakavyochochea ghasia.

Photo Credit
Maman Sidikou, Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Maqtaifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na mkuu wa MONUSCO.Picha:UM/Mark Garten